Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameutaka uongozi wa Kampuni ya Game Tracking Safaris(TGTS) kuangalia na kupitia nyaraka walizonazo ili kuona uhalali wa umiliki wa eneo la hekta 20000 kwenye vitalu tisa vilivyopo kwenye Ranchi ya Uvinza inayomilikiwa na Kampuni za Mifugo za Taifa (NARCO) kabla ya Selikali kuwatoa kwa nguvu ifikapo tarehe 1/1/2018.
Ametoa maelekezo hayo alipotembelea ranchi ya Uvinza kuangalia shughuli mbalimbali ambapo ametoa muda wa hadi Januari mosi mwakani.
Aidha Mpina amesema endapo Mwekezaji huyo ataendelea kubaki baada ya tarehe Mosi Januari, Serikali itamuondoa kwa nguvu na atatakiwa kulipa gharama zote za fidia na usumbufu.
“Ninakuagiza angalia taarifa mbalimbali ulizonazo kuhusu umiliki wa eneo hili kama utaona umeendelea kukaa hapa bila kufuata taratibu tafadhali uondoke mara mmoja ili kupisha Serikali kuendelea na shughuli zake,” amesema Mpina
Hata hivyo, amemuagiza Meneja Mkuu wa NARCO, Prof Philemoni Wambura kuwaandikia barua ya kuwaondoa wawekezaji wote katika Ranchi hiyo ambao hawajaendeleza kwa zaidi ya asilimia 40 na kwamba wawekezaji ambao wamewekeza kwa zaidi ya asilimia arobaini wanatakiwa kukamilisha malipo yote kabla ya Januari mosi mwakani.