Imeelezwa kuwa, utekelezaji wa mradi wa umeme wa bwawa la Mwl. Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha umeme wa Megawati 2,115 umefikia asilimia 80.2
Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, wakati wa utoaji wa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Amesema, “Kwa sasa utekelezaji wa mradi unaenda kwa kasi ambapo hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2022 umefikia asilimia 80.22, aidha mnamo tarehe 22 Desemba, 2022 zoezi la kuanza kujaza maji katika bwawa la JNHPP lilifanyika kwa kufunga mageti ya njia ya mchepusho.”
Akizungumzia ujazaji maji katika Bwawa hilo, Waziri Byabato amesema hadi kufikia Januari 16, 2023 kimo cha maji kilifikia mita 112.48 kutoka usawa wa bahari kutokea kimo cha mita 74 cha Desemba 22, 2022.
Aidha, ameongeza kuwa, utekelezaji wa mradi huo unaenda sambamba na mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa KV 400 kutoka eneo hilo hadi Chalinze – Pwani, na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Chalinze.
Tayari Serikali imeshalipa asilimia 74.7 ya malipo ya Mkandarasi na gharama za mradi huo ni shilingi Trilioni 6.5 na mradi huo unaendelea kutekelezwa kwa kasi ili asilimia za utekelezaji zilizobaki ziweze kukamilika kwa wakati.