Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watanzania kuitumia kampeni ya huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, kutoa taarifa kuhusu uwepo wa watu au vikundi vya watu ambao wanajihusisha na ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto.
Majaliwa ametoa wito huo hii leo Aprili 27, 2023 wakati akizindua kampeni hiyo ya miaka mitatu (Machi, 2023 – Desemba 2025), ikitarajia kuongeza uelewa wa sheria na upatikanaji haki, mifumo ya utoaji haki, masuala ya kisheria na haki za binadamu kwa kushirikiana na taasisi za serikali, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema, “kampeni hii pia itasaidia kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza, hususani wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu. Vilevile, itachangia kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato cha mmoja mmoja na kuleta utengamano wa kitaifa.”
Aidha, Waziri Mkuu poa ameongeza kuwa faida nyingine ya kampeni hiyo ni kusaidia kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika ngazi zote yaani kuanzia Serikali kuu hadi Serikali za Mitaa na kwamba ushiriki wa wadau wa huduma ya msaada wa kisheria utaongezeka kwa asilimia 80 katika ngazi za Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa.