Mjumbe wa Kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, John Heche amesema amewahi kupigiwa simu na mstaafu ambaye alimsimulia jinsi alivyotaka kujinyonga kwa kulipwa mafao yake Shilingi milioni 45 badala ya Shilingi milioni 100.
Heche ameyasema hayo wakati akiongea na Waandishi wa Habari jijini Dodoma, na kusema watu wengi wamejikuta wakiingia katika matatizo kutokana na kuhangaikia mafao yao bila mafanikio na hivyo kutoona faida ya utendaji kazi maishani mwao.
Amesema, “alinipigia simu nikapokea akasema yaani nafuatilia mafao yangu mwaka wa pili sasa halafu yanatoka badala ya kulipwa milioni 100 napewa milioni 45, mimi nataka kujinyonga, mnaweza ona sasa hivi pesa ya mtu unampangiaje matumizi mtu kafanya kazi miaka 30 anapewa 45 mbunge miaka 5 analipwa milioni 270 hii si sawa.”
Aidha, Heche ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo ni wazi kuwa Wafanyakazi wataacha kuwa waaminifu kwa kutafuta njia mbadala za kutengeneza maisha ikiwemo wizi kutokata na kukosa uhakika wa mafao pindi wanapostaafu.