Waziri wa Nishati, January Makamba amefanya ziara ya kikazi nchini Indonesia, yenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Taifa hilo katika sekta ya umeme, mafuta na gesi ambapo kujifunza jinsi ilivyopiga hatua kubwa ya kuwafikishia wananchi wake huduma ya Umeme kwa asilimia 99.9, licha ya kuwa na visiwa zaidi ya 1000.

Ziara hiyo, iliyofanyika Februari 9-10, 2023, Waziri Makamba kwa nyakati tofauti alikutana na Waziri wa Nchi anayeratibu biashara zinazomilikiwa na Serikali, Luhut Pandiaitan, Waziri wa Nishati na Rasilimali za Madini, Arifin Tasrif na Mwenyekiti wa Jukwaa la Biashara na Viwanda, Suryo Sulisto.

Wengine ni Rais wa Shirika la Umeme la Indonesia (PLN), Darmawan Prasodjo, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Mafuta ya Taifa ya Indonesia – Pertamina, Salyadi Sapurta, na Rais wa Kampuni ya Mafuta na Gesi ya MEDCO, Hilmi Panigoro.

Akiwa katika ziara hiyo, Waziri Makamba, aliongozana na Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Macocha Tembele, Kamishna na Petroli na Gesi, Michael Mjinja, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la TPDC Dkt. James Mataragio na maafisa wa Shirika la Umeme nchini – TANESCO na PURA.

Waziri Makamba ameeleza kuwa, ipo haja ya kuimarisha ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Indonesia katika suala la Umeme, mafuta na gesi na kuongeza kuwa, “Tanzania inahitaji kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa Nishati ya Umeme kwa wananchi wake.”

Kuhusu Mafuta na Gesi, Waziri Makamba ameupongeza uongozi wa kampuni ya Pertamina na kampuni yake tanzu ya Maurel and Prom inayofanya kazi Tanzania katika kitalu cha Mnazibay kwa kazi zote zinazoendelea.

Aidha, alimueleza mweyeji wake kuwa, kampuni hiyo inaweza kufanya vizuri zaidi kwenye uwekezaji wa kitalu hicho na kusema, “Serikali inatambua kitalu hicho bado kina rasilimali ya gesi nyingi zaidi ardhini, lakini uwekezaji wake hauridhishi.”

Ameongeza kuwa, “Serikali ya Tanzania inategemea sana uzalishaji wa gesi kutoka Mnazibay, ni vema Pertamina ikaliangalia jambo hili kwa kina kwa kushrikiana na mbia wake TPDC.”

Mara baada ya kikao hicho, Viongozi hao wa nchi mbili walikubaliana kusaini mkataba wa awali ya ushirikiano kati ya Wizara na Nishati ya Tanzania na Wizara ya Nishati na Rasilimali za Madini ya nchini Indonesia, katika kuendeleza miradi ya jotoardhi, usafirishaji wa umeme, utafutaji wa mafuta na gesi asilia na mafunzo ya kuongeza uwezo kwa wataalamu.

Jaribio ajali ya Ndege Kahama lazua Taharuki
TCRA kuzima laini za simu zisizo hakikiwa