Serikali nchini, ipo katika mchakato wa kubadilisha utaratibu mzima wa kutoa kazi kwa Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kwa kuzingatia zaidi watakaokidhi vigezo vya utekelezaji miradi kwa wakati na viwango.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na na Waziri wa Nishati, Januari Makamba wakati akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini (REA) ambapo pia ametoa muda wa miezi miwili kuanzia jana Januari 24, 2023, ili waitumie kurekebisha dosari na mapungufu yao, ili wafikie kiwango kinachotakiwa.

Waziri wa Nishati, Januari Makamba.

Amesema, “Serikali imewekeza fedha nyingi kutekeleza miradi hiyo haiwezi kukubali kuona Wananchi wakilalamika kutokana na kucheleweshwa kwa miradi husika na tupo katika mchakato wa kubadilisha namna ya kuwapa kazi, namna nzima tunatathmini hizi kazi na mwishowe hatima yenu kama Wakandarasi wa miradi ya REA.”

Aidha, Waziri Mkamba amefafanua kuwa Wizara kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), itafuata taratibu zote na kuhakikisha inawaengua ambao wanasababisha malalamiko huku akisisitiza watekelezaji duni zaidi na wasiobadilika Serikali pia itawashtaki kwenye Bodi ya Usajili wa Wahandisi (Contractors Registration Board), ili waondolewe katika orodha ya Wakandarasi wa Tanzania.

Mbali na maelekezo hayo, Waziri Makamba pia ameweka bayana kuwa lengo la Serikali ni kuwapa fursa wakandarasi wazawa lakini akatoa angalizo endapo wakishindwa kutimiza vigezo, basi Serikali haitasita kuwapatia kazi hizo Wakandarasi wa kimataifa waliothibitika kufanya kazi nzuri katika nchi mbalimbali.

Kikao hicho, kimehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wataalamu kutoka REA, TANESCO na Watendaji wa Wizara.

Bigirimana: Nimeondoka kwa salama na amani
Rais mstaafu kupandishwa kizimbani kwa ufisadi