Wakati mamilioni ya mashabiki hususan nchini Marekani na hata Eritrea wakiendelea kuomboleza kifo cha rapa Nipsey Hussle, Halmashauri ya jiji la Los Angeles inafanya mpango wa kubadili jina la mtaa mmoja kupewa jina la rapa huyo.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuanzishwa harakati kwenye mtandao inayotaka eneo ambalo Nipsey Hussle aliuawa kwa kupigwa risasi linalojulikana kama ‘Slauson Avenue na Crenshaw Boulevard kuitwa ‘Ermias Nipsey Hussle’.
Waratibu wa harakati hizo wamekusanya sahihi zaidi ya 480,000 zinazounga mkono uamuzi wa kufanya mabadiliko hayo kwa ajili ya kumuenzi rapa huyo aliyeuawa akiwa na umri wa miaka 33, nje ya duka lake la nguo la Marathon.
Nipsey anakumbukwa kwa uwezo wake mkubwa wa kurap, lakini pia kwa jinsi alivyokuwa akijihusisha na harakati za kupigania haki.
Mashabiki na wadau wa muziki watamuaga rasmi kesho, Alhamisi, Staples Center jijini Los Angeles. Tiketi za kushiriki tukio hilo ziliwekwa mtandaoni na ziliisha ndani ya dakika chache tu. Waratibu walitangaza kuwa tiketi hizo zimekwisha kabla ya saa moja tangu ziwekwe mtandaoni.
Hussle ambaye aliuawa Machi 31 mwaka huu, atazikwa Aprili 11, 2019. Wiki hii, albam yake ya ‘Victory Lap’ ilirejea tena kwenye chart za Billboard 200. Albam hiyo ilikuwa miongoni mwa albam zilizowania tuzo za Grammy mwaka huu katika kipengele cha Albam Bora ya Rap, lakini bahati ilimuangukia Cardi B na ‘Invasion of Privacy’.
Nipsey Hussle alikuwa rapa wa Marekani mwenye asili ya Eritrea, baba yake ni raia wa Eritrea aliyeingia Marekani akikwepa vita iliyokuwa ikiendelea nchini kwake. Rapa huyo alitembelea nchi hiyo mara kadhaa.