Uongozi wa Mtibwa Sugar umetamba kuibuka na ushindi katika mchezo wa Mzunguuko wa 23 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Dodoma Jiji FC.
Mtibwa Sugar itakua nyumbani Manungu Complex mkoani Morogoro kesho Jumamosi (Februari 11), ikipambania alama tatu za mchezo huo, huku ikiweka lengo la kupata alama tatu muhimu.
Afisa Habari wa Klabu hiyo iliyowahi kutwaa Ubingwa wa Tanzania Bara msimu wa 1998/99 na 1999/2000 Thobias Kifaru amesema, wanatambua mchezo huo utakuwa mgumu, lakini kikosi chao kimefanya maandalizi kabambe, ambayo yanawapa jeuri ya kuamini ushindi utapatikana.
“Wapinzani wetu wanakuja kwenye viunga vyetu vya mashamba ya miwa (Uwanja wa Manungu Complex), tunawajua wakulima wenzatu, ni vita ya dakika 90 ya kusaka alama tatu muhimu.”
“Wachezaji na Benchi la Ufundi wapo tayari kwa mchezo huo, Mashabiki nao wapo tayari kwa ajili ya kujitokeza Uwanjani kuishuhudia timu yao ikipambania alama tatu, ambazo zitatusogeza kwenye msimamo wa Ligi yetu.” amesema Kifaru
Baada ya michezo 22 Mtibwa Sugar ipo nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikijikusanyia alama 26, huku Dodoma Jiji FC ikikamata nafasi ya kumi kwa kumiliki alama 24.