Jeshi la Polisi Mkoani Katavi limesema mtu mmoja Heleni Nyankole (36), maarufu Beberu ameuawa kwa kupigwa risasi akidaiwa kuwa kinara wa kufanya mauaji ya kukodiwa.
Kamanda Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Ally Makame ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa Habari hii leo Julai 10, 2022 amesema mtuhumiwa Beberu aliuawa usiku wa kuamkia leo wakati wa akipambana na polisi.
“Marehemu Beberu alikuwa ni mkazi wa Kijiji cha Kapanga Wilaya ya Tanganyika, na anadaiwa kukodiwa ili kufanya mauaji ndani na nje ya Mkoa huo wa Katavi na ameuawa usiku wa kuamkia leo wakati akipambana na Polisi,” amesema Makame.
Kamanda Makame amefafanua kuwa June 28, 2022 majira ya usiku katika kijiji Bukombe mtuhumiwa huyo anadaiwa kumuua mkazi wa Kijiji hicho kilichopo Wilaya ya Tanganyika, Mandalu Ndulu (36), kwa kumkata shingoni na kitu chenye ncha kali.
Amesema, Beberu anadaiwa kutekeleza mauaji hayo baada ya kukodiwa na watu wawili wakazi wa kijiji cha Luhita kilichopo Bukombem kwa makubaliano ya kumlipa kiasi cha Shilingi laki nane (800,000), ili amuue mtu huyi Mandalu Ndulu.
Hata hivyo, baada ya Polisi kupata taarifa za tukio hilo waliwakamata watuhumiwa hao wawili na baada ya kuwahoji walikiri kumkodi mtuhumiwa huyo ambapo walimpa malipo ya awali Shilingi laki tatu (300,000), ili aweze kutekeleza mauaji hayo kwa makubaliano ya kumaliza kiasi kilichobaki baada kukamilisha kazi.
“Tulianza msako mkali Julai 7, 2022 usiku tulimkamata mtuhumiwa huyo wa mauaji kijiji cha Lwega kipo Wilayani Tanganyika akiwa amelala ndani ya nyumba yake, polisi walipomuamuru kujisalimisha lakini alikaidi,” amesimulia Kamanda Makame.
Amefafanua kuwa, “alipanda juu ya dari kisha kutoboa paa la nyumba iliyoezekwa kwa nyasi kwa kutumia panga, akiwa juu alijaribu kushuka ghafla akiwa na kipande cha nondo kwa lengo la kumjeruhi askari.”
Kufuatia kitendo hicho Kamanda Makame amesema askari waliokuwa katika eneo hilo walifyatua risasi hewani ili kumuonya lakini alikaidi na kuendelea kuwafuata ndipo risasi nyingine ilipofyatuliwa ikamjeruhi tumboni na alipoteza maisha wakati anakimbizwa Hospitalini.
Mtuhumiwa huyo Heleni Nyankole (Beberu), alikuwa akitafutwa na Jeshi la Polisi kwa muda mrefu kwa tuhuma za kukata watu mapanga katika maeneo tofauti ya ndani na nje ya Mkoa huo.