Imefahamika kuwa Uongozi wa Simba SC umetenga kiasi cha dola 150,000 (sawa na Sh 352,185,000) ili kumsajili kiungo mkabaji kutoka nchini Ethiopia na klabu ya St George, Yiech Gatoch Panom.
Simba SC imetenga kiasi hicho ili kufanikisha mpango wa kufanya maboresho katika kikosi chake, huku baadhi ya wachezaji wakitajwa kujiunga na timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao 2023/24 ambao umepangwa kuanza mwezi Agosti mwaka huu.
Kati ya nafasi ambazo Simba SC wamepanga kuziboresha kwa kusajili wachezaji ni safu ya kiungo mkabaji inayochezwa na Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude na Ismael Sawadogo.Mmoja wa mabosi wa Simba, amesema kuwa, tayari uongozi wa timu hiyo, wamepeleka ofa ya kumuhitaji kiungo huyo Yiech Gatoch Panom mwenye umbile kubwa kwa ajili ya kuimarisha safu hiyo ya kiungo.
Bosi huyo amesema tayari wameanza mazungumzo ya kumsajili kiungo huyo ambaye uongozi unaamini wakimpata, basi tatizo sugu Simba SC ofa la kiungo watalimaliza.
Ameongeza kuwa, uongozi wa St George tayari wameitangazia ya kumuachia kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28.
“Yapo maeneo mengi yenye upungufu katika timu yetu, ambayo ni lazima tuyafanyie maboresho, kati ya hayo ipo safu ya kiungo ya ukabaji na Panom ni kati ya wachezaji tuliokuwepo katika mazungumzo naye.
“Hivyo muda wowote tutakamilisha dili hilo la usajili, uzuri kwamba uongozi wa Simba upo tayari kutoa kiasi hicho cha pesa kuipata saini yake,” amesema bosi huyo.
Akizungumzia hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema: “Uongozi upo msituni ukijipanga kwa ajili ya usajili, kweli kabisa yapo baadhi ya majina ya wachezaji tupo nao katika mazungumzo ambayo kama yakienda vizuri tutamalizana nao.”
Panom amewahi kuzitumikia klabu za Wolaitta Dicha, Al-Anwar, Haras El Hodoud, Makelle City, Ethiopian Coffe, El Gouna na Anzhi Makhachkala ya Urusi.