Rais Uganda, Yoweri Museveni ameshutumu mauaji ya raia akiwemo Diwani, Mwanafunzi wa Chuo Kikuu na Mfanyakazi wa Serikali katika mazingira tofauti katika eneo la katikati ya jiji la Kampala.
Museveni, ameyasema hayo jijini humo na kudai kuwa, “Natupa lawama kwao na ninawalaani wauaji wa Kakooza, Diwani wa Kamwokya, mwanafunzi, Betungura, CAO kutoka Bukwo, Charles Ogwang na wengine na watalipa kama vile ADFs walivyokuwa wakilipa.”
Tayari, Polisi nchini Uganda wamemkamata mshukiwa mmoja wa mauaji ya Kakooza na watu wengine wanne akiwemo Mbunge wa Kassanda Kusini Frank Kabuye kuhusu mauaji ya Betungura na wengine wanne wanaohusishwa na mauaji ya kikatili ya Ogwang.
Hali ya usalama nchini Uganda kwa muda wa miezi miwili iliyopita, imetikiswa na wahalifu waliofanya matukio kadhaa ya mauaji na uhalifu, baadhi wakiwa na silaha ambao wamewatia hofu watu katika maeneo mengi.
“Wanadhani ni mzaha, hakuna mzaha mbaya kama kucheza kamari kwa kuua Waganda,” amesema Museveni saa chache kabla ya kutoa hotuba yake ya kitaifa hii leo Julai 20, 2022 inayotarajiwa kushughulikia mambo mbalimbali yanayolalamikiwa na Waganda milioni 44.
Katika taifa hilo la Afŕika Mashaŕiki, bei ya mafuta imekuwa ikipanda karibu kila siku – hadi kufikia Sh7,000– huku kukiwa na hali ngumu ya maisha ambayo inajitokeza zaidi kutokana na mfumuko wa bei na uhaba wa chakula nchini humo.
Julai 16, James Kakooza mwenye umri wa miaka 54 alipigwa risasi na kufa majira ya alfajiri na wahalifu waliokuwa kwenye pikipiki jijini Kampala, huku Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kikristo cha Uganda (UCU), Bewatti Betungura (25), akiuawa mapema mwezi huu.
Watu wengine 14, waliuawa kwa kuchomwa visu wakati wa kampeni ya uchaguzi katika Chuo Kikuu cha Makerere ikiwa ni wiki moja kabla ya wavamizi wengine walipiga risasi 26 na kuchoma moto gari na kumuua aliyekuwa afisa mkuu wa Wilaya ya Bukwo (CAO), Charles Ogwang.