Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amefanya mabadiliko katika Jeshi la Polisi na Wizara ya ulinzi kwa kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Jenerali Kale Kayihura na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Jenerali Henry Tumukunde.
Uamuzi huo wa Rais Museveni umekuja kufuatia mfululizo wa ripoti ya watu kuuawa na kutekwa huku hatua ya vyombo vya ulinzi ikionekana kusuasua.
Aidha, Museveni ambaye ametangaza uamuzi wake kupitia mtandao wa Twitter, amesema amemteua Okoth Ochola kuwa IGP na Jenerali Elly Tumwine kuwa Waziri wa Ulinzi.
Amewataka wananchi hususan vijana nchini humo kuelewa kuwa Serikali inafanya jitihada za kukomesha vitendo vya kihalifu vilivyoibuka nchini humo na kwamba mafanikio katika hilo “hayaji kwa miujiza bali kwa jitihada ambazo zinafanywa na Serikali yake.”
“Waganda, hususan vijana wadogo wanapaswa kufahamu kuwa ufumbuzi wa matatizo unajkuja kwa kufanya jitihada na sio kwa miujiza. Haya yote huchukua muda na jitihada,” alisema.
Ugandans, especially the young people, need to know that solutions to problems are not by miracles but by struggle and effort. These always take time and effort. The @NRMOnline , however, always succeeds because we are genuine and serious. We are not jokers and have never been.
— Yoweri K Museveni (@KagutaMuseveni) March 4, 2018
Alisisitiza kuwa kamera za CCTV zinapaswa kufungwa kwenye mitaa kwenye miji ili kupambana na uhalifu. Kauli hiyo ilikuja kufuatia ripoti ya kutekwa na kuuawa wanawake 24 katika jiji la Kampala na viunga vyake ndani ya kipindi cha miezi sita.
Rais Museveni alipaza sauti yake kufuatia kutekwa na kuuawa kwa msichana mwenye umri wa miaka 28, Susan Magara katika jiji hilo.