Tume ya Uchaguzi Uganda (EC) imemtangaza Yoweri Kaguta Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliofanyika Alhamisi tarehe 14 Januari 2021.
Kwa mujibu wa EC Museveni amepata kura 5,851,037 sawa na asilimia 58.64 ya kura zote zilizopigwa huku mpinzani mkuu wa Museveni, mwanamuziki Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, ameshika nafasi ya pili kwa kupata kura 3,475,398 ambazo ni sawa na asilimia 34.83 ya kura zote.
Bobi Wine hata hivyo alitangaza kutokukubaliana na matokeo hapo jana wakati EC ilipokuwa ikiendelea kutangaza matokeo.
Idadi kamili ya watu waliopiga kura ni 9,978,093 ikiwa ni sawa na asilimia 57.22 tu ya idadi ya watu waliojiandikisha kwenye daftari la wapiga kura hii ikiwa namaana kuwa zaidi ya asilimia 40 ya waliojiandikisha hawakujitokeza kupiga kura.
Rais Museveni, ambaye ana umri wa miaka 76 amekuwa madarakani kwa miaka 35 na ushindi huu unampa nafasi kuongoza kwa muhula wa sita kama Rais wa Uganda.