Matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais uliofanyika Alhamisi nchini Uganda yametolewa usiku wa kuamkia leo Januari 15, yakionyesha Rais Yoweri Museveni anaongoza dhidi ya mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi.

Tume ya Uchaguzi nchini humo imesema kuwa matokeo ya awali kutoka vituo visivyopungua 300 vya kupigia kura, yanaonesha Rais Museveni kutoka chama cha National Resistance Movement (NRM), amepata asilimia 61.3 huku Kyagulanyi maarufu Bobi Wine kutoka chama cha National Unity Platform (NUP) akiwa na asilimia 27.9 ya kura.

Ingawa inasemekana bado ni mapema ukilinganisha na vituo 300 vilivyohesabiwa kura kati ya vituo 34,000.

Tume ya Uchaguzi ya Uganda itachapisha matokeo mengine katika saa chache zijazo huku mshindi wa kiti cha urais anatarajiwa kutangazwa siku ya Jumamosi au Jumapili.

Katika upande mwingine wa Kinyang´anyiro kwenye uchaguzi huo ni nafasi za ubunge ambapo upinzani unaendelea kuleta changanmoto kwa wagombea wa chama tawala NRM.

Katika eneo la magharibi mwa Uganda uliko mji wa Hoima na ziwa Albert, wagombea wasiopungua sita wa upinzani wanaongoza katika kura zilizokwishahesabiwa dhidi ya wale wa chama tawala.

Kwa miaka mingi, eneo hilo halijawahi kuwa na mbunge kutoka chama cha upinzani isipokuwa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2016, wanasiasa wawili waliojiengua kutoka chama tawala NRM waliwania nafasi za ubunge kama wagombea binafsi na kuibuka na ushindi.

Kwa sehemu kubwa, matokeo kamili ya nafasi za ubunge yanatarajiwa kutangazwa leo Ijumaa na kutoa picha kamili ya uwakilishi katika Bunge linalokuja.

Simba kufunga usajili na Chikwende
Kaze aliwahofia Chama, Miquissone