Aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Lusubilo Mwakabibi na mwenzake Edward Haule, mratibu wa mradi wa uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka wakati wa utumishi wao

Mwakabibi na mwenzake wamefikishwa Mahakamani leo Agosti 20, 2021 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi na jopo la mawakili watatu waandamizi wa Serikali, wakiongozwa na Mshanga Mkunde mbele ye hakimu mkazi mwandamizi, Evodia Kyaruzi.


Aidha Wakili Martin, mbele ye hakimu mkazi mwandamizi, Evodia Kyaruzi amedai katika shtaka la kwanza ni matumizi mabaya ya ofisi, tukio wanalodaiwa kutenda kati ya Machi 2020 na Machi 2021 katika Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Inadaiwa kuwa siku hiyo, Mwakabibi na Haule wakiwa waajiriwa wa Manispaa hiyo, katika utekelezaji wa ardhi walielekeza ujenzi wa stendi ya mabasi eneo la Buza katika kiwanja kinachomilikiwa na Dayosisi ya Kanisa la Anglikana bila kuwa na ruhusa.


Shitaka la pili ni matumizi mabaya ya madaraka, tukio wanaodaiwa kutenda Machi 2020 na Machi 2021 katika eneo hilo, washtakiwa kwa makusudi wanadaiwa walitumia madaraka yao vibaya kinyume na kifungu cha 3(1) Cha Sheria ya Ardhi na kifungu cha 3,4,5,7 na 11 cha Sheria ya Ardhi ya mwaka 2019.

Hata hivyo Wakili Mshanga amedai upelelezi haujakamilika na hivyo kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Wakati huo huo upande wa utetezi ukiongozwa na Jeremiah Mtobesya na Benedict Ishabakaki umeomba Mahakama itoe dhamana kwa washtakiwa hao kwa kuwa, mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao hayajataja kiasi cha fedha katika hati ya mashtaka.

Hakimu Kyaruzi baada ya kusikiliza maombi hayo, ametoa masharti ya dhamana dhidi ya washtakiwa, ambapo amesema kila mshtakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Shilingi milioni 10.

Pia washtakiwa wanatakiwa kuwasilisha fedha taslimu milioni kumi au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo, kutoruhusiwa kutoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kuwa na kibali cha Mahakama, pamoja na kuwasilisha hati za kusafiria.

Aidha,Hakimu Kyaruzi baada ya kueleza hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 2, 2021

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Augusti 21, 2021
Balozi Mulamula atoa angalizo kwa wanadiplomasia