Uongozi wa klabu ya Young Africans umejipanga kuhakikisha wanafanya vizuri kweye michezo iliyosalia pale ligi itakaporejea, huku wakipiga hesabu kali katika michuano ya kombe la shirikisho (ASFC), iliyofikia hatua ya robo fainali.
Makamu Mwenyekiti wa Young Africans Fredrick Mwakalebela amesema wamepokea kwa furaha tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli kuwa anaweza kuruhusu mashindano mbalimbali ya soka nchini kuendelea, endapo atashauriwa na wataalamu wake na kuona kuna haja ya kutoa agizo la kuendelea kwa ligi.
Amesema Young Africans inasubiri tamko la TFF kufahamu ni lini michuano hiyo itarejea lakini wao wamejipanga kufanya vizuri kwani hata wakati huu ambao ligi imesimama, nyota wao wanafanya mazoezi kikamilifu.
“Tumelipokea kwa furaha tamko la Rais, sasa tunajipanga kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye ligi na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ili kupata nafasi ya uwakilishi wa kimataifa mwakani” “Tunawasubiri TFF waseme lini tunaanza ili tujipange rasmi ila wachezaji wetu wanaendelea na mazoezi kama walivyoelekezwa,” alisema Mwakalebela
Kimahesabu Young Africans ina nafasi finyu ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu wakiwa wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo, wakikusanya alama 51 ambazo ni alama 20 pungufu ya vinara wa ligi hiyo Simba.
Hata hivyo Young Africans wanaweza kujihakikisha tiketi ya kushiriki michuano ya kombe la Shirikisho msimu ujao kama wataweza kutwaa taji la shirikisho (ASFC) wakiwa wametinga hatua ya robo fainali
Droo ya hatua hiyo itafanyika Serikali itakaporuhusu kurejea kwa ligi na mashindano mengine.