Hatimaye Bondia Hassan Mwakinyo amefunguka kuhusu kuachana na kocha wake, Hamis Mwakinyo aliyemnoa kwa muda mrefu hadi alipokuwa kwenye 15 bora ya dunia kwenye uzani wake.

Tangu pambano lake Dodoma, kumekuwepo na taarifa za Mwakinyo kuachana na kocha huyo ambaye pia ni kaka yake, ikielezwa sababu za kutoendelea naye ni masuala binafsi.

Mmoja wa watu wa karibu wa bondia huyo, amesema Mwakinyo sasa hayupo na kocha huyo kutokana na masuala binafsi ya nje ya ngumi.

“Kuna vitu havikuwa sawa kati yao, hivyo sasa Mwakinyo hayupo na kocha wake, ndiyo sababu hata pambano la Dodoma alikuwa na (second) msaidizi wa ulingo ambaye ni kocha mwingine.”

Amesema, Mwakinyo alitofautiana na kocha wake hata kabla ya pambano la Dodoma, hali iliyosababisha kujifua chini ya kocha mwingine na kwenye pambano hilo Aprili 23 alipomchapa Kuvesa Katembo alikuwa na kocha tofauti na Hamis.

Ingawa Hamis hakupatikana kuzungumzia hilo, Mwakinyo amesema hajaachana na kocha huyo, japo ni kweli hakuwa na kocha huyo kwenye pambano lake la Dodoma hivi karibuni.

“Yeye alibaki Tanga, alikuwa na majukumu mengine, ndiyo sababu sikuweza kusafiri naye, lakini bado ni kocha wangu, sijaachana naye na nitaendelea kuonekana naye kwenye mapambano yangu yajayo,” amesema.

Ingawa taarifa kutoka Tanga zinasema kuna mpango wa promota, Ally Mwazoa kuwakutanisha ili Mwakinyo arudi kwa kocha wake wa muda mrefu.

“Mwakinyo ndiye alizingua, ugomvi na kocha wake ni wa kawaida kabisa, hataki awe na ukaribu na watu ambao yeye Mwakinyo hapatani nao, jambo ambalo haliwezekani, lakini Mwazoa ni kama anataka hilo liishe, kuna mkakati wa kuwapatanisha ili Mwakinyo arudi kwa kocha wake.”

“Hamis ametoka mbali na bondia huyo, hadi anakwenda kumpiga Sam Eggington kule Uingereza na kuwa nyota alikuwa chini yake,” alisema mmoja wa watu wa karibu wa bondia huyo.”

Hivi sasa Mwakinyo ni wa 59 kwenye viwango vya ubora duniani katika uzani wake na wa nne Afrika akipoteza nyota moja na nusu kati ya nne alizowahi kumiliki.

Madini yamesaidia ukuaji wa uchumi kwa jamii, Taifa - Dkt. Kiruswa
Jeshi EAC limeshindwa kupambana na waasi - Tshisekedi