Uongozi wa klabu ya Coastal Union umesema kwamba mchezaji Bakari Nondo Mwamnyeto ataendelea kuhudumu katika klabu hiyo msimu ujao kwa sababu wameshindwa kupata muafaka kamili na uongozi wa Yung Africans ambao wameonyesha nia ya kumsajili.
Mjumbe wa kamati ya utendaji ndani ya klabu hiyo Hussein Ally amesema kwamba Young Africans ndio klabu pekee hadi sasa iliyofika kwenye uongozi wa klabu hiyo ili kukamilisha usajili wa Mwamnyeto, lakini swala hilo limeshindikana baada ya mchezaji kukataa dau la klabu hiyo ambalo ni shilingi milioni sitini.
Ally amesema kwamba mchezaji husika anahitaji dau la shilingi milioni mia moja,jambo ambalo limeonekana kuwa gumu kwa klabu hiyo yenye maskani yake makuu jijini Dar es salaam.
Amesema kwamba wao kama Coastal Union swala hilo wameliacha kwa mchezaji mwenyewe licha ya kusalia na mkataba wa mwaka mmoja wa kuendelea kuhudumu kwenye klabu hiyo ya mkoani Tanga.
Wakati huo huo inaelezwa kuwa endapo Young Africans itakamilisha dili la usajili wa Bakari Nondo Mwamnyeto, huenda wakasitisha mpango wa kumleta nchini beki kutoka nchini Kenya Mussa Mohammed.