Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), limemtaja mwamuzi atakayechezesha mchezo wa fainali wa Kombe la Dunia, Ufaransa dhidi ya Croatia, utakaoshuhudiwa kwenye uwanja wa Luzhniki nchini Urusi, Jumapili hii.
Nestor Pitana ambaye ni raia wa Argentina mwenye uzoefu, ndiye atakayepuliza kipyenga ndani ya dimba Jumapili hii ikiwa ni mechi yake ya tano nzito kwenye Fainali za Kombe la Dunia.
Pitana mwenye umri wa miaka 43 amepata nafasi hiyo kutokana na historia yake ya kumudu mechi ngumu, akianza na mechi ya ufunguzi kati ya wenyeji Urusi na Saudi Arabia kwenye uwanja huohuo.
Anakuwa mwamuzi wa pili kutoka Argentina kuchezesha mechi kubwa zaidi kwenye ulimwengu wa Soka akimfuatia Horacio Elizondo aliyeweka rekodi mwaka 2006.
Pitana alikuwa kwenye jopo la waamuzi kwenye Fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil miaka minne iliyopita, na hii itakuwa mechi ya tano, akiwa na rekodi nzuri alipochezesha mchezo wa robo fainali kati ya Ufaransa na Uruguay.
Wadau wa soka wamemteta Pitana, wengi wakionekana kumkubali kutokana na historia yake nzuri.
Mchezaji wa Croatia, Ivan Rakitic amemzungumzia Pitana akikumbuka alivyoumudu mtanange kati ya kikosi cha timu yake dhidi ya Denmark kwenye hatua ya mzunguko wa timu 16.
“Nilifurahi kusikia atakuwa mwamuzi wa fainali. Tulikuwa na bahati kumuona akichezesha mchezo kati yetu na Denmark. Sio tu kwamba tulishinda lakini alikuwa vizuri. Wasaidizi wake pia walikuwa wazuri sana,” amesema Ivan Rakitic.
Pitana atasaidiwa na waamuzi wa pembeni Hernan Maidana na Juan Pablo Belatti. Massimiliano Irrati wa Italia atasimamia upande wa uamuzi wa kutumia video, Video Assistant Referee (VAR).