Mwanachama na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya NCCR- Mageuzi, George Kahangwa ametangaza kujivua uanachama wa chama hicho na kujiweka pembeni kwa kile alichodai kuwa NCCR-Mageuzi ni chama kilichogubikwa na giza nene.
Dk Kahangwa ambaye ni msomi wa masuala ya elimu ametangaza uamuzi huo kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Facebook ikiwa ni kipindi ambacho kumekuwa na wimbi la wanasiasa wa upinzani kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Mniwie radhi kuwataarifu hili. Sioni dalili yoyote ya mwanga katika chumba cha giza nene linaloigubika NCCR- Mageuzi. Hivyo, hiari ileile niliyoitumia kujiunga, sasa naitumia kukaa pembeni,” amesema Dk Kahangwa katika ujumbe aliouweka Facebook.
Hata hivyo, Mkuu wa Oganaizesheni na Utawala wa NCCR-Mageuzi, Florian Mbeo amethibitisha kujiondoa kwa Dk Kahangwa.
“Ni kweli amejivua uanachama, alikieleza chama kuhusu suala hilo na hata leo asubuhi nimezungumza naye. Uamuzi aliochukua ni wa kawaida tunauheshimu,” amesema Mbeo.
Hata hivyo Kuhangwa alitafutwa ili kutoa uthibitisho wa kukihama chama hicho, simu yake haikupatikana.