Mwandishi wa habari wa Citizen TV, Jacque Maribe (pichani) anayetuhumiwa kuhusika katika mauaji ya mfanyabiashara mwanamke, Monica Kimani jijini Nairobi amerudishwa rumande kwa amri ya Mahakama.
Mahakama ya Kiambu, Kaskazini mwa Nairobi leo imepitisha ombi la upande wa mashtaka la kutaka Maribe aendelee kushikiliwa rumande kwa siku 11 zaidi wakati upelelezi ukiendelea.
Mwendesha mashtaka alifanikiwa kuishawishi mahakama kuwa endapo mtuhumiwa ataachiwa huru anaweza kuharibu upelelezi unaoendelea. Alieleza kuwa tayari wameshachukua vinasaba vya mtuhumiwa na sampuli kwenye nyumba ya marehemu lakini bado wanaendelea kukusanya vielelezo.
Mwandishi huyo ambaye alikuwa mtangazaji wa habari, alikamatwa Jumamosi iliyopita ikiwa ni siku kadhaa tangu taarifa ya kuuawa kwa Monica zilipotangazwa, habari ambayo yeye pia aliitangaza kama ‘Breaking News’.
Maribe alikamatwa siku chache baada ya mpenzi wake Joseph Irungu ambaye ndiye mtuhumiwa namba moja kukamatwa.
Mwili wa marehemu Kimani ulikutwa katika bafu la nyumba yake iliyoko Kilimani jijini Nairobi, ukiwa na alama za kunyongwa shingoni na alama za kipigo cha mikono mgongoni.
Taarifa za awali za upelelezi zilieleza kuwa Irungu alijipiga risasi akiwa ndani ya chumba cha mpenzi wake (Maribe) lakini alipona, ikiwa ni saa chache tangu kutokea kwa tukio la mauaji ya Monica. Polisi wameeleza kuwa kuna uhusiano wa karibu kati ya tukio hilo la kujaribu kujiua na mauaji ya Monica.
Maribe, Irungu na washtakiwa wengine wanaohusishwa na tukio hilo wanaendelea kusota rumande.