Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Kenya ametaka Tume Huru ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC) kuchunguzwa ili kubaini kama ilijihusisha na uvunjifu wa sheria katika uchaguzi mkuu uliopita.
Mkurugenzi wa Mashtaka wa nchi hiyo, Keriako Tobiko amevitaka vyombo vya usalama ikiwa ni pamoja na jeshi la polisi na taasisi ya kuchunguza rushwa kuichunguza IEBC na watumishi wake.
Tobiko aliitaka vyombo hivyo pia kuchunguza tuhuma dhidi ya maafisa wawili waandamizi wa IEBC kuwa waliweza kuingia kwenye mfumo wa kielektroniki wa Tume hiyo kinyume cha sheria na kuchakachua matokeo.
Mahakama Kuu nchini humo ilifuta uchaguzi uliofanyika Agosti 8 mwaka huu na kueleza kuwa uligubikwa na udanganyifu, hivyo kupoteza sifa za kuwa uchaguzi huru na wa haki.
Kupitia uamuzi huo ilibatilisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta wa asilimia 54 dhidi ya mshindani wake mkuu, Raila Odinga kwa mujibu wa IEBC na kuagiza uchaguzi mwingine kufanyika ndani ya siku 60.
Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Oktoba 17 mwaka huu.