Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kheri James amesema umoja huo uko tayari kuomba radhi kwa mambo ambayo yalitokea huko nyuma, kama yapo, ili kuweka jukwaa safi kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama hicho jijini Dodoma, James amesema kuwa huu ni wa kati wa vijana kushikamana na kuondoa tofauti zinazoweza kusababisha umoja wao kutetereka.
“Yawezekana katika siasa zetu na hekaheka zetu tuliweza kutofautiana kimitazamo, yapo mambo ambayo huko nyuma yalipelekea umoja wetu ukaterereka, UVCCM hatuoni aibu kusema tunaomba radhi kwa hayo kama tuliyatenda na tupo tayari kurekebisha ili kutengeneza jukwaa safi kwa Rais wetu kuanza upya akiwa na Watu walioshikamana na kuwa wamoja ili Nchi yetu iweze kwenda mbele” amesema.
Mwenyekiti huyo wa UVCCM amesema kuwa vijana wa chama hicho wana imani kuwa Rais Samia Suluhu ataliongoza vyema taifa.