Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amewataka mashabiki wa Young Africans kuachana na suala la kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison kwa kuwa Mshambuliaji kutoka DR Congo Heritier Makambo anarudi Jangwani.
Nchemba ametoa kauli hiyo mjini Dodoma, huku tetesi za kurudi kwa Makambo zikishika kasi katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu huu 2020/21.
Young Africans wamekua na mpango mkakati wa kuhakikisha wanamrudisha Morrison ambaye alitimkia Simba SC mwanzoni mwa msimu huu, kwa kutangaza hadharani bado wanamtambua kama mchezaji wao halali.
“Mashabiki na Wanachama waachane kabisa na kelele za Morisson kwa sasa, Young Africans ina mpango kabambe wa kumsajili tena Mshambuliaji Heritier Makambo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa.” amesema Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba.
Taarifa zinasema kuwa Young Africans itasajili washambuliaji wawili wazuri ukiwa ndio mpango namba moja wa mabosi wa timu hiyo iliyo chini ya Kocha Nasreddin Nabi, na jina la Makambo linaonekana kuzidi kung’aa katika msako wa mabosi hao wa klabu hiyo ambayo usiku wa jana ilikuwa uwanjani kuvaana na Mwadui katika mechi ya Ligi Kuu.
Utamu ni kwamba Makambo ni kama amechoka maisha ya Guinea akiwa na klabu ya AC Horoya iliyomnunua miaka mitatu iliyopita akitokea Young Africans na sasa yuko tayari kurejea tena Jangwani kuendelea kuwajaza kama alivyofanya wakati akikiwasha chini ya kocha Mwinyi Zahera.
Young Africans inaamini Makambo anaweza kuja kuwasaidia kwa kuwa anajua vyema mazingira na falsafa ya soka lao na kikubwa zaidi wako mabosi wengi wanaona ni bora kuchukuliwa mkongomani huyo kuliko kuja na mtu mpya asiyejua mazingira ya soka la klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.