Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema kutokana na ubora wa kikosi Simba SC, alitegemea wangefika fainali Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu 2020/21.
Dk Mwigulu ambaye ni Mwanachama na Shabiki wa klabu ya Young Africans, ameyasema hayo mjini Dodoma, ambapo amesisitiza wazi kuwa watani zao wa jadi wa kikosi imara.
Amesema aliamini Simba SC wangeweza kufika fainali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, lakini kilichowakwamisha ni kujiandaa zaidi na mchezo dhidi ya Young Africans, badala ya michezo ya Kimataifa.
“Kwa kweli wapinzani wetu Simba SC wana kikosi imara na chenye ubora, walikua na kila sababu ya kucheza fainali kwenye michuano ya kimataifa msimu huu, lakini walibugi ‘Step’ kuifikiria sana Young Africans, na kusahau majukumu yao kimataifa.”
Simba SC ilitupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwenye hatua ya Robo Fainali, kwa kufungwa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini jumla ya mabao manne kwa matatu.
Mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Afrika Kusini Simba SC ilikubali kufungwa mabao manne kwa Sifuri, kabla ya kushinda mabao matatu kwa sifuri kwenye mchezo wa mkondo wa pili, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Simba SC ilimaliza hatua ya Makundi ikiwa kinara wa kundi hilo, lililokuwa na vigogo kama Al Ahly ya Misri, Al Merreikh ya Sudan na AS Vita Club ya DR Congo.
Kwenye hatua za awali Simba SC ilifanikiwa kuzitoa Plateau United ya Nigeria kwa jumla ya bao moja kwa sifuri, kisha wakaibanjua FC Platnums ya Zimbabwe mabao manne kwa moja.