Beki wa kulia wa Young Africans, Kibwana Shomari amesema yupo tayari kupigania namba na mchezaji yeyote atakayesajiliwa klabuni hapo, kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu na michuano ya Kimataifa.

Shomari ametangaza utayari wa kuwania nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Young Africans, kufuatia taarifa za kusajiliwa kwa beki wa kulia kutoka DR Congo na klabu ya AS Vita Club Djuma Shaaban.

Shomari amesema jukumu lake kubwa ni kuhakikisha anaisaidia Young Africans, hivyo anavyosikia taarifa za kusajiliwa kwa mchezaji mwingine klabuni hapo, anaamini kuna haja ya kuendelea kupambana ili kuiwezesha klabu hiyo kufikia lengo iliyojiwekea.

Hata hivyo beki huyo amesema ujuo wa Djuma utamfunza mambo mengi, kutokana na uzoefu wake kwenye michuano ya kimataifa, akiwa na AS Vita Club ya DR Congo.

“Nasikia Djuma Shabani amesaini Young Africans na tutakuwa naye msimu ujao, ni jambo zuri kwa sababu anakuja kuboresha timu yetu.”

“Binafsi nimefurahi sababu nitajifunza vitu vingi kutoka kwake kutokana na uzoefu alionao, lakini sihofii kukosa nafasi ya kucheza sababu mwenye jukumu la kupanga timu ni kocha,” amesema Shomari

Mlinzi huyo ambaye alijiunga na Young Africans akitokea Mtibwa Sugar, amesema kucheza nafasi moja na wachezaji wakubwa kama huyo ni faida kwake hasa ikitokea anamuweka benchi hawezi kuchukia wala kufikiria kuondoka.

Kuvaa barakoa amri Hospitali ya Taifa Muhimbili
Mwigulu Nchemba: Simba SC ingecheza fainali CAF