Mwongozo wa maandalizi ya mpango na Bajeti ya mwaka 2023/24 umewaelekeza Maafisa Masuuli kuzingatia masuala ya Jinsia, wakati wa uandaaji, uwasilishaji, utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini pamoja na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa Mpango na Bajeti zao.
Haya yamebainishwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA) Halima Mdee aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaanza kutengeneza bajeti kwa jicho la jinsia.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande.
Alisema, pamoja na maelekezo hayo, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake – UN Women, inaendelea kushirikiana na Serikali kujenga uwezo katika maandalizi ya nyaraka za sera kwa kuzingatia masuala ya kijinsia.
Aidha Chande amebainisha kuwa, katika mwaka 2022/23, Wizara ya Fedha na Mipango imeunda kikosi kazi kwa ajili ya kuboresha mwongozo wa maandalizi ya mipango na bajeti ya Serikali kwa jicho la kijinsia na hivyo kuwa imefanikisha uanzaji wa suala hilo muhimu.