Mabao yaliyofungwa na Juan Arce na Marcelo Moreno yameisaidia Bolivia kuzima ndoto za Argentina kuendeleza wimbi la ushindi kwenye michezo ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia ukanda wa Amerika ya Kusini.
Bolivia wamepata ushindi huo, ikiwa saa kadhaa baada ya kufungiwa kwa mshambuliaji Lionel Messi ambaye anategemewa na kikosi chake cha Taifa.
Messi alimbwatukia na kumtolea lugha chafu mwamuzi aliyechezesha mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Uruguay, ambapo Argentina walichomoka na ushindi wa bao moja kwa sifuri lililofungwa na mshambuliaji huyo wa FC Barcelona.
Maamuzi ya kufungiwa michezo minne yaliyotolewa na FIFA, yalitangazwa saa sita kabla ya mchezo dhidi ya Bolivia.
Kufungwa kwa Argentina kumeendelea kuwaweka kwenye wakati mgumu wa kufuzu fainali za kombe la dunia za 2018, licha ya kushika nafasi ya tano kwenye msimamo wa kundi la kusini mwa Amerika lenye timu kumi.
Bolivia wamefikisha point kumi ambazo zinawaweka kwenye nafasi ya tisa.
Matokeo ya michezo mingine ya kundi la kusini mwa Amerika iliyocheza leo alfajiri.
Ecuador 0 – 2 Colombia
Chile 3 – 1 Venezuela
Brazil 3 – 0 Paraguay
Peru 2 – 1 Uruguay
Ukanda wa kusini mwa Amerika kusini hutoa timu nne zinazofuzu moja kwa moja katika fainali za kombe la dunia, na timu itakayomaliza nafasi ya tano hucheza mchezo wa mchujo dhidi ya timu kutoka ukanda wa Oceania.