Mkuu wa Benchi la Ufundi la Young Africans Nasreddine Nabi ametangaza vita ya mapambano kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ihefu FC, utakaochezwa Alhamis (Julai 15).
Kocha Nabi amesema dhumuni kubwa la kutangaza vita ya mapambano kuelekea mchezo huo, limetokana na changamoto alizokutana nazo kwenye mchezo dhidi ya Mwadui FC, ambao kikosi chake kilipata ushindi wa mbinde kwa mabao 3-2 dakika za lala salama, Uwanja wa Benjamin Mkapa mwishoni mwa mwezi Juni.
“Kama benchi tunajua hauwezi kuwa mchezo rahisi, tuliona ugumu tuliopata kwa Mwadui licha ya kwamba ilikwishashuka daraja, hivyo hatuwezi kuwabeza hata kidogo Ihefu na tutaingia tukiwa kamili,” amesema Nabi.
Kocha huyo kutoka nchini Tunisia, amekuwa na rekodi nzuri tangu alipojiunga na Young Africans April 19, baada ya kucheza mechi tisa, sita za Ligi Kuu na tatu za Kombe la Azam, ameshinda saba, kufungwa moja na sare moja.
Young Africans inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 70, ikitanguliwa na Simba SC iliyotawazwa kuwa mabingwa mara nne mfululizo jana Jumapili (Julai 11), baada ya kuifunga Coastal Union mabao 2-0, hali iliyoiwezesha kufikisha alama 79.