Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Nasreddine Nabi amesema bado kuna kazi kubwa ya kufanya, kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, ili kufikia ndoto za kucheza Robo Fainali.
Young Africans juzi Jumapili (Februari 19) ilipata ushindi wake wa kwanza Hatua ya Makundi, kwa kuifunga TP Mazembe ya DR Congo 3-1, baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa kufungwa 2-0 na US Monastir ya Tunisia.
Kocha Nabi amesema Kikosi chake kilionesha uwezo mkubwa kisoka dhidi ya TP Mazembe na kilipaswa kushinda, lakini hiyo haitoshi kufanya waamini watacheza Hatua ya Robo Fainali msimu huu.
Amesema bado ataendelea kufanya kazi yake ya kupunguza kama si kuyaondoa baadhi ya mapungufu kwenye kikosi chake, ili kukifanya kuwa bora na kushinda michezo inayofuata.
“Inaonesha kundi letu ni gumu kwa sababu kila mtu ana alama, hivyo bado tunaangalia nini cha kufanya katika michezo itakayotukabili siku za usoni.”
“Sio ushindani wa kusema tumemaliza, kwani bado nitaendelea kuyafanyia kazi mapungufu nilioyaona kwenye kikosi chetu, ili tufikie malengo ya kuvuka hatua ya makundi na kucheza Robo Fainali,” amesema Kocha Nabi
Young Africans itaendelea na Mchaka Mchaka wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika Hatua ya Makundi mwishoni mwa juma hili, kwa kucheza ugenini nchini Mali dhidi ya Real Bamako.
Mchezo huo wa Mzunguuko wa Tatu utapigwa Jumapili (Februari 26), katika Uwanja wa Machi 26 mjini Bamako, saa kumi jioni kwa saa za Mali.
Mwamuzi Joshua Bondo kutoka nchini Botswana, ametajwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ kuchezasha mchezo huo.