Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa wito kwa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kuzingatia mamlaka yake ili kuepukana na malalamiko ya nchi wanachama ya kuingilia uhuru wa ndani wa nchi hali inayopelekea baadhi ya Nchi Wanachama kuondoa matamko ya kujiweka chini ya mamlaka ya Mahakama hiyo huku baadhi zikisita kuridhia Mkataba ulioanzisha Mahakama hiyo.

Dkt. Mpango ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Mwaka wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na watu, jijini Arusha na kuongeza kuwa changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi ni pamoja na zile za kusikiliza na kutolea hukumu mashauri ambayo yako nje ya mamlaka ya mahakama hiyo, Mahakama kutoa hukumu dhidi ya nchi wanachama bila kuzingatia mazingira na mifumo ya kisheria ya nchi za Afrika na kupelekea kutotekelezeka.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango.

Amemesema, njia ya mazungumzo kati ya Mahakama na Nchi Wanachama inapaswa kutumika ili malengo yaliyokusudiwa ya Mahakama hiyo yaweze kufikiwa na kumpongeza Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Imani Aboud, kwa hatua anazochukua kuimarisha mahusiano kati ya Mahakama hiyo na Nchi Wanachama na kumsihi kuendeleza jitihada hizo.

Makamu wa Rais amesema Tanzania ina dhamira ya dhati kutekeleza malengo ya Umoja wa Afrika na utekelezaji wa Ajenda 2063 pamoja na kushiriki katika kujenga Taasisi imara za Afrika ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Afrika.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Mahakama ya Afrika
ya Haki za Binadamu na Watu Jaji Imani Aboud na Makamu wake Jaji Blaise Tchikaya, Majaji wa Mahakama hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro, Majaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki pamoja na Viongozi mbalimbali mara baada ya Ufunguzi wa Mwaka wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu uliofanyika Makao Makuu ya Mahakama hiyo mkoani Arusha.

Amesema kwa kutambua wajibu wa kuhamasisha na kutetea haki za binadamu, Tanzania imeendelea kuwa chini ya mamlaka ya Mahakama ya Haki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu pamoja na kusaini na kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa ya haki za binadamu.

Kwa upande wake, Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jaji Imani Aboud amesema ni vigumu kwa malengo ya Umoja wa Afrika ya Ajenda 2063 kufikiwa bila kuwepo msingi imara wa haki za
binadamu kwani ustawi, umoja, utangamano, maendeleo, ulinzi na usalama pamoja na utangamano katika jumuiya za kimataifa unafungamanishwa na haki za binadamu.

Wanajeshi 51 wauawa kwa shambulio la kushtukiza mpakani
Nabi: Bado kuna kazi kubwa Kimataifa