Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, masijala ndogo ya Mbeya, imemhukumu Keneth Mwamwaja kifungo cha maisha jela, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukutwa na kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine gramu 248.91.

Hukumu hiyo, imetolewa na Jaji Yose Mlyambina baada ya kujiridhisha kuwa upande wa mashitaka ulithibitisha mashataka dhidi ya Mwamwaja pasipo kuacha shaka yoyote.

Akisoma huku hiyo, Jaji Mlyambina alisema hukumu hiyo ilizingatia hoja za majumuisho za pande zote pamoja na maombi ya upande wa utetezi ikiwa ni pamoja na kudai kuwa mshtakiwa alikuwa ni mkosaji kwa mara ya kwanza, aliwekwa mahabusu kwa miaka zaidi ya minne, ni kijana mdogo wa miaka 37 na nguvu kazi ya taifa, pia ana familia inamtegemea.

“Nimefikiria majumuisho ya pande zote na maombi ya upande wa utetezi, pia nimepitia vifungu vya sheria ya udhibiti wa za dawa za kulevya ambayo inaelekeza kuwa mtu yeyote anayetiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya atahukumiwa kifungo cha maisha,” alisema.

“Katika hali hiyo ninamhukumu mshtakiwa Mwamwaja kwenda jela maisha kuanzia Februari 6, 2023 kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya kama sheria inavyoamuru,” alisema.

Katika kesi hiyo upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi watano na vielelezo sita na upande wa utetezi walipeleka mashahidi watatu akiwemo mshtakiwa bila kielelezo chochote na wakati wa kusikilizwa kesi ilidaiwa kuwa Juni 2, 2019 katika eneo la Jakaranda B mkoani Mbeya, mshtakiwa alikutwa akisafirisha dawa hizo za kulevya.

TANESCO yapokea mashine umba ya kwanza
Wanne mikononi mwa Polisi kwa ujangili