Kiungo kutoka nchini Ubelgiji, Nacer Chadli amekamilisha taratibu za kujiunga na AS Monaco ya Ufaransa, akitokea West Brom ya England kwa ada ya Pauni milioni 10.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29, amekamilisha uhamisho huo na kusaini mkataba wa miaka mitatu, ambao utamuwezesha kuitumikia klabu yake mpya hadi mwaka 2021.
Chadli, ambaye aliisaidia timu ya taifa ya Ubelgiji kumaliza katika nafasi ya tatu wakati wa fainali za kombe la dunia, ameondoka nchini England baada ya kuwasilisha ombi kwa uongozi wa West Brom kufuatia kikosi cha Darren Moore kushuka daraja mwishoni mwa msimu wa 2017/18, kutoka ligi kuu hadi ligi daraja la kwanza.
Chadli ameiambia tovuti ya asmona, “nina furaha ya kujiunga na AS Monaco, ni klabu kubwa kwa Ufaransa, ni miongoni mwa klabu zitakazoshiriki ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu huu.”
“Matokeo ya msimu uliopita, yanadhihirisha klabu hii ni klabu ya aina gani, ninatarajia kushirikiana na wachezaji wenzangu ili kuendelea kusaka mafanikio ziadi, kwa msimu huu. Nitajitahidi kufanya kila jambo zuri kwa ajili ya kuisaidia AS Monaco, ili ifikie malengo yake mwishoni mwa msimu huu,” aliongeza.
Chadli alijiunga na West Brom akitokea Tottenham mwaka 2016, na hadi anaondoka klabuni hapo alikua ameshacheza michezo 38, na mara kadhaa alikabiliwa na changamoto za kupata majeraha.
Licha ya kujiuguza mara kwa mara, Chadli alibahatika kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ubelgiji kilichoshirii fainali za kombe la dunia, na alikua sehemu ya kiosi kilichoanza wakati wa mchezo wa robo fainali dhidi ya Brazil na kisha Ufaransa katika hatua ya nusu fainali.