Mgombea urais wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad ameonyesha wasiwasi wa kukwamishwa katika kuwania kinyang’anyiro hicho.
Akizungumza katika kongamano la vijana wa ACT Wazalendo, lililofanyika visiwani Zanzibar, leo Septemba 8, Maalim Seif amedai kuwepo kwa baadhi ya watu wa vyama vingine ambao wamepanga kumuwekea pingamizi katika tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ili asiteuliwe kugombea.
Maalim Seif amesema, anawakaribisha watu wanaotaka kumuwekea pingamizi akisema kuwa anafahamu namna ya kupangua pingamizi zao.
“Nasikia kuna watu washapangwa na vyama vingine kuniwekea pingamizi, nawakaribisha kwa sababu kuniwekea pingamizi, atakuja kutoa hoja zake na ushahidi wake, na mimi naujua vilevile,” amesema Maalim Seif.
” Sioni kama kuna pingamizi yoyote, kama itasimama juu yangu, mimi nimezaliwa Mtambwe hamjui ninyi? Ndiyo sifa ya kwanza ya mgombea urais, awe Mzanzibari wa kuzaliwa sio Mzanzibari mkaribishi,” ameongeza Maalim Seif.
Kwa mujibu wa ratiba ya ZEC, zoezi la uchukuaji na urudishaji fomu za kugombea urais, lilifunguliwa tarehe 26 Agosti 2020, na linatarajiwa kufungwa leo Septemba 6, 2020.