Klabu ya Chelsea huenda ikamnyakua aliyekua Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich Julian Nagelsmann, ambaye anahusishwa na Tottenham baada ya Antonio Conte kufukuzwa kazi.

Nagelsmann alishtua vichwa vya habari Ulaya baada ya Uongozi wa FC Bayern Munich kumtimua mwishoni mwa juma lililopita, huku kocha huyo akitajwa kuwa bado ni miongoni mwa makocha bora Ulaya, taarifa zikiripoti mwenyekiti wa Tottenham, aliwasiliana naye.

Aidha, Gazeti la Dail Mail limeripoti Tottenham huenda ikapata upinzani kutoka kwa Chelsea katika mbio za kuwania saini ya Nagelesmann.

Imeripotiwa Nagelsmann anakubalika ndani ya viunga vya Stamford Bridge kwa sababu atakuwa mrithi mzuri wa Graham Potter aliyekalia kuti kavu.

Lakini hiyo itategemea matokeo mazuri ambayo Chelsea itapata kabla ya mwishoni mwa msimu kwa sababu mmiliki wa klabu, Todd Boehly anataka mabadiliko makubwa ya uongozi.

Kwa kuongezea, Tottenham huenda ikapata ushindani kutoka Real Madrid, endapo Carlo Ancelotti atafukuzwa kazi baada ya kuboronga msimu huu.

Chelsea imeendelea kujitutumua kwenye ligi baada ya kufanikiwa kutinga Robo Fainali ya Ligi Mabingwa Ulaya itacheza dhidi ya Real Madrid huku kibarua cha Potter kikiwa hatarini.

Hata hivyo Uongozi wa The Blues umeweka wazi utampa muda kocha huyo baada ya usajili wa nguvu walioufanya wakati wa Dirisha Dogo la usajili mwezi Januari 2023.

PICHA: Simba SC yawasili Casablanca-Morocco
Ruvu Shooting haitaki kushuka daraja