Wawakilishi wa Tanzania Bara kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAF) Namungo FC itapambana dhidi ya El Hilal El Obeid ya Sudan katika raundi inayofuata ya michauno hiyo.
Namungo FC imepenya kwenye hatua hiyo, baada ya kuiondoa kirahisi Al Rabita FC ya Sudan Kusini, kufuatia mchezo wa mkondo wa pili uliopangwa kuchezwa Jumapili (Desemba 06) kufutwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Namungo ilishinda kwa mabao 3-0, mawili yalifungwa na Steven Sey na moja Shiza Kichuya, hivyo Al Rabita iliomba mechi ya marudiano ichezwe tena hapa nchini kutokana na uwanja wao kuwa katika matengenezo ili kukidhi viwango vya CAF.
Mchezo wa kwanza utashuhudia Namungo FC wakianzia nyumbani kati ya Desemba 22-23, na mchezo wa mkondo wa pili utachezwa nchini Sudan ambapo El Hilal El Obeid watakua wenyeji kati ya Januari 5-6, mwakani.
Katibu wa Namungo FC, Suleiman Ally, amesema baada ya kumfahamu mpinzani wao kwenye hatua inayofuata, wameanza mikakati ya maandalizi ili kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza ambao utachezwa Dar es salaam, kabla ya mchezo wa pili kuchezwa Sudan.
“Baada ya kumjua mpinzani wetu, tumekaa na kocha wetu kuweka mikakati ili kufanya vizuri na kusonga mbele zaidi,” amesema Suleiman Ally.
Endapo Namungo itaitoa El Hilal El Obeid katika raundi hiyo inayofuata, bado itakabiliwa na kucheza mchezo wa mchujo nyumbani na ugenini dhidi ya timu mojawapo itakayopangiwa nayo kutoka zile zitakazotolewa kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa na endapo itapata matokeo ya jumla ndipo itatinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.