Uongozi wa Klabu ya Namungo FC umepanga kumsainisha mkataba mpya kocha wao kutoka nchini Rwanda Hitimana Thierry, ili aendelea kukinoa kikosi cha klabu hiyo ya mkoani Lindi.
Mkataba wa sasa wa kocha huyo utafikia kikomo mwezi Juni mwaka huu, na tayari ameanza kuhusishwa na mipango ya kunyakuliwa na klabu nyingine za ligi kuu Tanzania bara.
Msemaji wa klabu hiyo inayoshiriki ligi kuu ya soka Tanzania bara kwa mara ya kwanza msimu huu wa 2019/20, Kindamba Namlia amesema uongozi una mipango madhubuti na kocha huyo, na tayari umeshaanza kuchukua hatua za kumsainisha mkataba mpya.
Kindamba amesema mipango ya kumsainisha mkataba mpya kocha Hitimana, ilianza kusukwa kabla ya mlipuko wa janga la virusi vya Corona, na kama isingelikua tatizo hilo, basi hii leo mambo yangelikua tayari yameshakalishwa.
“Ni kweli mkataba na kocha Hitimana unaelekea ukingoni lakini tupo tayari kumuongezea mpya kwa kuwa bado ni muhimu kwetu, na kama isingekuwa hili janga la Corona tungekuwa tumeshamuongezea mkataba.”
Kindamba ameongeza kuwa kocha Hitimana ni mtu muhimu kwenye timu yao na wanaona kama wameokota dhahabu mchangani, hivyo hawatokubali kuiachia kirahisi.
Mpaka ligi inasimama mwezi uliopita Hitimana alikuwa ameiongoza Namungo kufika nafasi ya nne kwenye msimamo baada ya kufikisha alama 50.