Mwimbaji wa kike, Nandy anayefanya vizuri na ngoma yake ‘Wasikudanganye’ amekumbushia changamoto alizokutana nazo wakati anagonga hodi kwenye ulimwengu wa Bongo Fleva akiwa na ndoto ya kuwa msanii mkubwa.
Msanii huyo amesema kuwa kitu ambacho hawezi kusahau ni kitendo cha kuvunjiwa CD ya nyimbo zake za awali na mdau mkubwa wa muziki nchini, Ruge Mutahaba alipomfuata akimuomba amsaidie kusimamia kazi zake.
Nandy ameiambia XXL ya Clouds FM kuwa kitendo hicho kilimfanya aanze kufikiria kuwa kuingia kwenye tasnia ya muziki sio rahisi kwani Ruge alimtaka kuachana na nyimbo zake zote na kuanza upya.
- Makala:Hongera ‘Maua Sama’ kwa mchango wako kwenye muziki wa Hip-hop nchini
- Vanessa Mdee aungana na Maua Sama kutikisa
“Nakumbuka wakati nimetoka Nigeria kwenye mashindano [Tecno Own The Stage] nilimfuata Bosi Ruge ili anisaidie, akanambia ‘kalete nyimbo zako’. Nilipompelekea akaniuliza ‘uko tayari kuanza upya?’ nikajibu ndio. Basi akavunja CD mbele yangu,” Nandy amefunguka.
Nandy alianza kujitengenezea mashabiki baada ya kuwakilisha Tanzania katika mashindo ya kutafuta vipaji vya kuimba ya ‘Teckno Own The Stage’ yaliyofanyika nchini Nigeria ambapo aliibuka mshindi wa pili.