Madarasa mapya na jengo moja la maktaba ya shule ya msingi Kijitoupele, wilaya ya Magharibi ‘B’, Mkoa wa Mjini Magharibi Visiwani Zanzibar yamejengwa na kukamilika ndani ya kipindi cha wiki moja na siku mbili.

Ujenzi huo uliomshangaza Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein na kupongeza utekelezaji wake, umefanywa kwa ushirikiano wa nguvu za wananchi, wadau wa elimu na Serikali kupitia kampeni ya Mimi na Wewe inayoratibiwa na Mkuu wa Mkoa huo, Ayoub Mohamed Mahmoud (pichani).

Akizungumza katika mahojiano maalum na Dar24 mkoani humo, Mkuu huyo wa Mkoa wa Mjini Magharibi alisema kuwa ujenzi huo wa muda mfupi ulitokana na agizo lake pamoja na kuhusisha wataalam, wananchi wenyewe kushiriki moja kwa moja lakini kikubwa zaidi ni yeye kushiriki na kusimamia kwa karibu ujenzi huo.

“Siku ya kwanza nilishiriki mwenyewe asubuhi hadi jioni, kuanzia siku ya pili nilikuwa nakwenda almost (karibu) kila siku kukagua na kuona tumefikia wapi, tumekwama wapi, tutatue nini,” aliiambia Dar24.

“Kwahiyo kunahitaji kwa namna fulani kujitoa. Lazima ujitoe, kama huwezi kujitoa huwezi kujenga kwa haraka,” aliongeza.

Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Maghari, Ayoub Mohamed Mahmoud baada ya kuweka jiwe la msing kwenye jengo la shule ya msingi Kijitoupele

Akizungumza wakati wa majumuisho ya ziara yake ya siku tatu katika mkoa huo, Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein alimpongeza mkuu huyo wa mkoa kwa juhudi zake kupitia kampeni hiyo.

“Nimeona nguvu ya ‘Mimi na Wewe’ pale Kijitoupele. Umenieleza kuwa shule ile imegharimu shilingi milioni 76.1. Hamuwezi kuamini, shule ile imejengwa kwa muda mfupi, haraka na imekamilika vizuri na tumeizundua ndani ya siku 11,” alisema Dkt. Shein.

Aidha, Dkt. Shein alipongeza juhudi zilizofanywa na mkuu wa mkoa kupitia kampeni hiyo kuchangia damu iliyosababisha upatikanaji wa damu zaidi katika hifadhi ya damu (blood bank) iliyoko eneo la Sebuleni.

Kampeni ya Mimi na Wewe ilizinduliwa mwezi Mei mwaka huu na Mkuu huyo wa Mkoa kwa lengo la kuboresha maisha ya jamii hususan vijana.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa mkoa, kupitia kampeni hiyo, vijana zaidi ya 50 waliokuwa wameathirika na dawa za kulevya wamepelekwa kwenye vituo maalum vya matibabu (sober house) na pia vijana 11 wamewezeshwa kuachana na tabia za ushoga.

Video: Sheikh Ponda afunguka maiti 15 kwenye viroba, Lugumi mambo mazito
Magazeti ya Tanzania leo Agosti 22, 2017