Kiungo mpya wa Klabu ya Simba SC Nassoro Kapama ameingia katika mzozo na viongozi wa klabu hiyo, kufuatia suala la kuwa mbioni kutolewa kwa mkopo kwa masharti ya kupunguziwa mshahara wake.
Kapama alisajiliwa Simba SC akitokea Kagera Sugar kwa makubaliano ya mkataba wa miaka miwili, ambao unamuwezesha kulipwa mshahara wa Shilingi Milioni nne kila mwezi.
Taarifa kutoka ndani ya Simba SC zinaeleza kuwa Uongozi wa klabu hiyo umemtaka Kapama kupunguziwa Mshahara wake kutoka Milioni nne hadi Milioni Moja ili atolewe kwa Mkopo, kufuatia Kocha Mkuu Zoran Maki kumuengua kwenye mipango yake.
Hata hivyo Kapama amegoma kukubali sharti hilo, huku akisistiza yupo tayari kuondoka klabuni hapo kwa mkopo na kuendelea kulipwa Mshahara wa Shilingi Milioni nne, ama avunjiwe mkataba wake na kwenda kusaka nafasi kwenye klabu nyingine katika kipindi hiki ambapo Dirisha la Usajili bado lipo wazi.
“Kapama hana shida, yupo tayari kwenda popote kwa mkopo, lakini sharti lake ni kuendelea kulipwa Mshahara ule ule ambao alikubaliana na viongozi wa Simba SC wakati akisajiliwa miezi miwili iliyopita.”
“Suala kubwa hapa ni kutaka kutoa nafasi kwa mchezaji lakini mkanganyiko upo kwenye maslahi yake ya kila mwezi, unajua Kocha Mkuu Zoran Maki amemuengua Kapama kwenye mipango yake, hivyo analazimika kuondoka kwa mkopo ama mkataba wake kuvunjwa katika kipindi hiki, ili awahi kusajiliwa na klabu nyingine kabla ya kufungwa kwa Dirisha la usajili mwishoni mwa mwezi huu.” Kimeeleza chanzo cha taarifa kutoka ndani ya Simba SC.
Akizungumzia sakata hilo Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema suala hilo lipo kiutendaji zaidi, hivyo hana mamlaka ya kusema chochote zaidi ya kusubiri taarifa kutoka kwa viongozi wa juu.
“Hilo suala ni la kiutendaji, hivyo tuwaachie wao ndio wanajua nini cha kufanya, mimi nitakapopewa taarifa rasmi nitavifahamisha vyombo vya habari.” amesema Ahmed Ally
Nassoto Kapama bado hajapata nafasi ya kuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC kilichocheza michezo minne tangu kiliporejea nchini kikitokea Misri kilipokua kimeweka kambi mjini Ismailia.
Simba SC ilicheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya St George ya Ethiopia, kisha ikakutana na Young Africans kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii kabla ya kuanza Mshike Mshike wa Ligi Kuu kwa kupapatuana na Geita Gold FC na Kagera Sugar.