Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema amefarijika na jinsi zoezi la sensa ya watu na makazi lilivyoanza mwaka huu na kupokelewa katika maeneo mbalimbali nchini huku akiwatoa hofu Wananchi ambao hawajafikiwa na Makarani.

Majaliwa, ametoa kauli hiyo Agosti 23, 2022 mara baada ya kumaliza kuhojiwa na karani wa sensa nyumbani kwake kijiji cha Namahema, kata ya Nandagala, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.

Amesema anawashukuru viongozi wakuu wa Kitaifa akiwemo Rais, Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa hamasa walizotoa wakati wa zoezi zima la kuhamasisha umma.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na Karani wa Sensa aliyefika Nyumbani kijiji cha Namahema, kata ya Nandagala, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, kwa ajili ya zoezi la kuhesabiwa.

Aidha Majaliwa kuwa sensa ya mwaka huu ni ya aina yake kwa sababu inajumuisha uratibu wa mfumo wa anuani za makazi ambao haukuwepo kwenye sensa tano zilizotangulia na pia inaenda kwa mifumo ya kidigitali ambapo mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHEMA), inatumika.

“Awamu tano zilizopita huyu karani hapa angekuwa na makaratasi mengi ya madodoso kibao lakini kutokana na mfumo huo ana kifaa kimoja tu ambacho kimebeba maswali yote. Mimi hapa nimejibu maswali 100 ndani ya muda mfupi kwa kutumia kifaa hicho,” amefafanua Waziri Mkuu.

Hata hivyo, amewataka wananchi ambao hawajafikiwa na makarani kutokuwa na hofu kwani sensa hii ina maswali madogomadogo ambayo hayalengi kuleta tafrani bali kupata taarifa za kuisaidia nchi kupanga mipango ya kujiletea maendeleo.

Nassoro Kapama aigomea Simba SC
Kenya: Malema amuita Odinga wamuunge mkono Ruto