Baada ya kukiongoza kikosi cha Taifa Stars kuitoa Burundi katika mchezo wa kusaka tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia 2022, kocha mkuu wa mabingwa wa kombe la shirikisho (ASFC) Azam FC Etienne Ndayiragije, amesema kwa sasa anahamishia nguvu kwa Triangle United FC ya Zimbabwe.
Azam FC watacheza dhidi ya Triangle United FC katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika Septemba 15 mwaka huu, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kocha Ndayiragije amesema, baada ya kukamilisha kazi ya kuivusha Taifa Stars, hana muda wa kupoteza kutokana na hitaji la upande wa klabu anayoitumikia, la kuhakikisha wanapata matokeo mazuri, hasa ukizingatia wataanzia nyumbani na baadae kumalizia ugenini.
“Tumebakiza siku chache, Septemba 15 ni karibu mno, nimeshajiunga na timu yangu tangu jana jumatatu, nimeshaanza kushirikiana na wenzangu katika benchi la ufundi ili kufanikisha kusudio letu la kupata ushindi dhidi ya Wazimbabwe.
“Tunawafahamu wapinzani wetu, tumeshawafuatilia na kuwaangalia wakicheza katika michezo kadhaa kwa njia ya televisheni,” alisema kocha huyo kutoka nchini Burundi.
Hata hivyo Kocha Ndayiragije amekiri mchezo wao dhidi ya Triangle United FC hautakuwa rahisi, lakini akaendelea kusisitiza kuwa, maandalizi yanayoendelea uwanaani Aam Complex, Chamazi yatakua silaha tosha ya kuhakikisha wanapata ushindi nyumbani.
Azam FC walifuzu kucheza hatua ya mzunguuko wa kwanza wa kombe la shirikisho Afrika, baada ya kuwatoa Fasil Kenema ya Ethiopia, kwa jumla ya mabao matatu kwa mawili.