Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imejibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wadau kuhusu sababu zilizochangia mwitikio mdogo wa wananchi kujitokeza kupiga kura tofauti na idadi ya watu waliojiandikisha.
Ufafanuzi huo umetokana na idadi ya wapiga kura waliojitokeza katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kinondoni na Siha uliofanyika Februari 17 pamoja na chaguzi nyingine za hivi karibuni za ubunge na udiwani.
Ambapo Katika jimbo la kinondoni kati ya wapiga kura 264,066 waliojiandikisha ni wapiga kura 45,454 tu ndio waliofika kupiga kura, huku Siha kati ya waliojiandikisha 55,313 waliopiga kura ni 32,277.
Akijibu hoja hiyo Naibu Katibu Uendeshaji Uchaguzi wa NEC, Irene Kadushi amesema mwitiko wa wapiga kura unaathiriwa na tabia ya watu kuhama chama kimoja na kisha kuruhusiwa kugombea nafasi ile ile katika chama alichohamia, amesema hii inachangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa idadi ndogo kwa wapiga kura.
Mnamo 02/12/2017, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya Civic United Front – (CUF), Maulid Said Abdallah Mtulia aliamua kujivua uanachama wa chama hicho na kuhamia CCM, huku Disemba 14, 2017, Mbunge wa Jimbo la Siha kwa tiketi ya CHADEMA, Godwin Ole Mollel alijiuzulu nafasi hiyo pamoja na uanachama wa CHADEMA na kujiunga na CCM.
Na viongozi hao hao kupewa tena nafasi hizo kugombea majimbo hayo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM ,vyama ambavyo wamehamia, hii imetajwa kuwa moja kati ya changamoto kubwa inayorudisha nyuma mwitikio wa wananchi kupiga kura zao.
Aidha ameeleza kuwa miaka ya nyuma hilo halikuwa changamoto sana , bali changamoto ilikuwa ni fedha katika utoaji elimu ya mpiga kura, lakini tatizo hilo limepatiwa ufumbuzi wa kutosha na sasa elimu ya mpiga kura ni endelevu.
Pia amesisitiza kwamba kwa sasa hakuna taasisi yeyote inayoingilia shughuli za NEC katika utendaji wake ikiwemo serikali ambayo jukumu lake huishia kwenye kuipatia tume fedha kwa ajili ya shughuli zake.