Tume ya taifa ya Uchaguzi imesema kuwa wabunge wanawake wa viti maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA) waliteuliwa kwa kuzingatia taratibu zote za kikatiba na kisheria kupitia orodha iliyowasilishwa na chama hicho.
Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt.Wilson Mahera, amesema wabunge wa viti maalum wa CHADEMA waliteuliwa kwa kuzingatia taratibu zote kikatiba na kisheria kupitia orodha ya majina ya wanachama waliopendekezwa iliyowasilishwa na Katibu mkuu wa chama hicho kupitia barua yake.
Kupitia taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt.Wilson Mahera Charles, ambayo imeeleza kuwa katibu wa Chadema aliwasilisha orodha ya majina ya wanachama wanaopendekezwa kuteuliwa katika nafasi hiyo katika barua yenye kumb. Na.C/HQ/ADM/20/TU/05/141.
Dkt. Mahera amesema Tume ilipokea barua ya CHADEMA tarehe 19/11/2020 na kuteua wabunge na madiwani wanawake wa viti maalum kwa kuzingatia matakwa ya katiba na sheria tarehe 20/11/2020
Taarifa hii ya Tume inakuja kufuatia madai ya CHADEMA juu ya wabunge wake walioapishwa bila kufuata taratibu na kanuni za sheria.