Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali nchini kuyafikia maeneo ya Wananchi kwa ajili ya kutoa huduma, kusikiliza kero zao na kuzitatua.
Biteko ameyasema hayo katika Kijiji cha Nyakanazi Wilaya ya Biharamulo Mkoani Kagera, akiwa njiani kuelekea Wilayani Ngara kuwasha umeme Vijijini pamoja na kuhudhuria Mkutano wa Mawaziri wa Nishati kutoka nchi za Tanzania, Burundi na Rwanda wanaohusika na Mradi wa umeme wa Rusumo utakaozalisha megawati 80.
Amesema, “tutoke maofisini na tuwafuate wananchi walipo, haina maana yoyote kama kuna kiongozi hapa na kuna shida ipo na haijawahi kutatuliwa, Mhe, Rais anachotaka ni wananchi hawa kusikilizwa na kama kuna kero sisi tuzimalize kabla yeye hajaja.”
Aidha, Dkt. Doto Biteko pia ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuwa na mpango maalum wa kusambaza umeme kwenye eneo hilo la Nyakanazi kutokana na kupitiwa na miundombinu ya umeme kutoka kituo kikubwa cha umeme cha Nyakanazi ambacho kinasambaza kwenye maeneo mengine ya nchi.