Israel ipo katika maandalizi ya kuapishwa kwa serikali mpya ambayo itamfanya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuwa upande wa upinzani baada ya miaka 12 madarakani na uwepo wa mzozo wa kisiasa katika chaguzi nne ndani ya kipindi cha miaka miwili.
Tayari Naftali Bennett kutoka chama cha Yamina ameapishwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Israel na kumaliza utawala wa miaka 12 wa Netanyahu.
Iwapo Bennett akitaka kuendelea kudumu katika nafasi yake hiyo atapaswa kudumisha umoja wa vyama vya kisiasa na vyama vingine vya mirengo ya kulia, kushoto na kati.
Netanyahu, ambae anakabiliwa na mashitaka ya rushwa atasalia kuwa kiongozi wa chama kikubwa bungeni na anatarajiwa kuipinga vikali serikali mpya.
Serikali mpya ya Israel imeahidi kurejesha hali ya kawaida baada ya sintofahamu ya miaka miwili iliyotokana na chaguzi nne, siku 11 ya vita vya Gaza mwezi uliopita na kadhia ya janga la corona ambalo imeuvuruga uchumi wa taifa hilo kabla haijadhibitiwa kwa kiasi kikubwa na kampeni iliyofanikiwa ya chanjo.
Viongozi mbalimbali duniani wamemtumia salamu za pongezi waziri mkuu mpya wa Israel Naftali Bennett aliyechukua wadhifa huo baada ya Bunge la nchi hiyo kuidhinisha serikali mpya ya mseto ya vyama vya upinzani.
Salamu hizo za pongezi zinafuatia ushindi mwembamba uliopatikana katika bunge la Israel siku ya Jumapili ambao umemwezesha Naftali Bennett, mwanasiasa kutoka chama kidogo cha Yamina, kuchukua wadhifa wa waziri mkuu chini ya serikali ya mseto ya vyama nane vya siasa na kumaliza enzi ya uongozi wa Benjamin Netanyahu.
Serikali ya Bennet imeidhinishwa kwa ushindi wa kura moja tu baada ya kuridhiwa na wabunge 60 huku ikipingwa na wabunge 59 katika bunge lenye viti 120 ambapo Mbunge mmoja alijizuia kupiga kura.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amempongeza Bennet kwa kuapishwa kuiongoza Israel na kumuahidi kuwa serikali yake itafanya naye kazi katika suala la usalama wa Israel na kutafuta amani kwenye kanda ya Mashariki ya Kati.
Salamu sawa na hizo zimetolewa na Rais Joe Biden wa Marekani ambaye amesema Washington inasalia kuwa mshirika mkuu na muhimu wa Israel na itaendelea kuiunga bila kutetereka.
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya, Charles Michel, Kansela Sebastian Kurz wa Austria na Mawaziri Wakuu wa Uingereza na Canada nao pia wamepongeza Bennet kwa ushindi alioupata Bungeni na kuwa Waziri Mkuu.