Mkurugenzi wa soka wa mabingwa wa Ufaransa Paris Saint Germain, Leonardo, ameendelea kuweka msukumo wa kutaka kuona mshambuliaji Neymar akiondoka klabuni hapo, baada ya dili la uhamisho wake wa majira ya kiangazi kufeli.
Neymar alihusishwa na mipango ya kutaka kurejea FC Barcelona wakati wa dirisha la usajili mwezi uliopita, lakini taratibu za uhamisho wake zilishindikana kufuatia baadhi ya makubaliano ya pande hizo mbili kukwama.
Taarifa kutoka jijini Paris zinaeleza kuwa, Leonardo amepanga kuufufua mpango wa kuuzwa kwa Neymar wakati wa dirisha dogo la usajili (mwezi Januari), huku akiamini kwa kipindi hicho kutakua na uwezekano wa kupata klabu itakayofikia makubaliano ya kumsajili.
Sababu kubwa ya kiongozi huyo kutaka Neymar kuondoka PSG zinatajwa kuwa, ni kushindwa kumudu gharama za mshahara wake kwa juma, ikilinganishwa na mchangano hafifu anaoutoa klabuni hapo.
Hata hivyo mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, pia aliwahi kuhusishwa na mpango wa kutaka kusajiliwa na Real Madrid, lakini bado harakati hizo ziligonga mwamba.
Wakati huo huo baba wa Neymar, amekiri kupokea taarifa za mwanawe kuendelea kupata changamoto ya kuondoshwa PSG, kwa kusema lolote litakaloafikiwa, atakubaliana nalo ili kumuwezesha mtoto wake kuwa na furaha wakati wote.
Neymar Senior amesema kusudio lake kubwa ni kutaka kuona mtoto wake akicheza soka na kufurahia maisha, tofauti na sasa ambapo kila kukicha amekua katika vyombo vya habari akizungumzwa kuhusu uhamisho wake.
Neymar alijiunga na PSG mwaka 2017 akitokea FC Barcelona kwa dau la Pauni milioni 222, na tayari ameshawatumikia mabingwa hao wa Ufaransa katika michezo 37 ya ligi na kufunga mabao 34.