Faisary Ahmed – Kagera.
Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Toba Nguvila amewaagiza maafisa Elimu wa Wilaya, Waratibu Elimu ngazi ya Kata na Wakuu wa Shule kwa kushirikiana na wazazi, kuweka mipango itakayowezesha wanafunzi watahiniwa kupata chakula shuleni na kuongezewa muda wa masomo ili kuwawezesha wanafunzi hao kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya mwisho.
Nguvila ameyasema hayo wakati akiwa kwenye kikao cha Elimu – REM, cha robo ya pili ya mwaka cha kuthaminisha utendaji kazi na maendeleo ya usimamizi wa taaluma, kilichofanyika katika Manispaa ya Bukoba.
Amesema, “wanafunzi wote wa madarasa ya mitihani wapate chakula shuleni bila kukosa na pili kuwepo na mipango ya mwisho wa wiki za mafunzo mgango na wafanye mitihani yenye hadhi ya kitaifa.”
Kwa upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Kagera, Kharifa Shemahonge amesema wanatarajia kuwa na mitihani mwezi huu (Julai), na Jumatatu (Julai 24, 2023), wataanza na kidato cha pili, huku Maafisa elimu wa kata, Anitha Mashulano na Ausoni Revelian wakieleza utayari wao utakaosaidia kuinua taaluma ya Mkoa wa Kagera.
Katika majadiliano yao, viashiria 22 vya ufanisi -KPI, vyenye malengo 18 mojawapo la lengo la Mkoa wa Kagera ni kutoka ufahulu wa asilimia 65 kwa tathmini ya matokeo ya majaribio na kufikia zaidi ya asilimia 85 ya ufahulu kwa mwaka huu wa 2023 kwenye matokeo ya mitihani ya Taifa.