Baada ya kukamilisha zoezi la uchaguzi mkuu na kumpata Rais wa serikali ya awamu ya tano pamoja na wabunge, hivi sasa maswali makuu mawili yanayosubiri majibu ni nani atakayekuwa waziri mkuu na nani atakayekuwa Spika wa Bunge la Kumi, huku jina la aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa likiibuka tena kwa nafasi ya uspika.

Edward Lowassa na Samwel Sitta

Edward Lowassa na Samwel Sitta

Kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa na gazeti moja kubwa nchini, licha ya kuhamia Chadema, timu ya Edward Lowassa bado iko katikati ya wabunge wateule wa CCM ambao walikuwa wanamuunga mkono wakati akiwa katika chama hicho.

Imeelezwa kuwa wabunge waliokuwa ‘Team Lowassa’ bado ni wengi na wana imani naye hadi sasa na kwamba tamko la Dkt. Magufuli kupambana na wanafiki wanaokihujumu chama hicho kwa kuwapa siri wapinzani imechochea nguvu ya timu hiyo kwani wanaamini wao ndio walengwa. Hivyo, wanapanga kumchagua Spika wa Bunge atakayewaokoa baadhi yao dhidi ya mkono wa Rais wa serikali ya awamu ya tano.

Lowassa na Pinda

Taarifa hizo zimeeleza kuwa watu wa ndani wa CCM wamedokeza kuwa timu hiyo imepanga kuwa endapo Dkt. Magufuli atakahitaji wabunge hao wamsaidie katika masuala ya bunge, basi Spika huyo atamuomba pia asiwaadhibu baadhi ya watu walioko kwenye timu hiyo wanaochukuliwa kama wasaliti.

Tayari majina ya makada wakongwe wa CCM yameanza kutajwa kuwania nafasi hiyo ikiwa ni pamoja na Samwel Sitta aliyekuwa Spika wa Bunge la 9, Anne Makinda aliyekuwa Spika wa Bunge la Kumi pamoja na Mussa ‘Zungu’ Azzan. Wengine ni Dkt. Emmanuel Nchimbi na Mathias Chikawe.

Kwa mujibu wa sheria, Spika wa Bunge anaweza kuchaguliwa kati ya wabunge au watu ambao wana sifa za kuwa wabunge.

Kwa mujibu wa taratibu za CCM, Kamati Kuu ya chama hicho itapendekeza majina matatu yatakayopelekwa bungeni kupigiwa kura.

Wakati hayo yakiendelea, kesho (Novemba 5), Dkt. John Magufuli ataapishwa na kuwa rais wa serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Tanzania Ya Viwanda Kuanza Rasmi Leo, Dunia Kushuhudia Kiapo Cha Magufuli
Faidha Kuyaanika Maisha yake na Sugu