Watanzania wameaswa kupenda kufanya mazoezi ya mara kwa mara  ili kuepuka ugonjwa wa kisukari na viashiria vyake  katika jamii.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Neema Rusibamayila alipomwakilisha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa kuadhimisha siku ya Kisukari duniani yaliyofanyika jana jijini Dar es salaam.

“Watanzania tunatakiwa kupenda kujijengea tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuweza kuepuka magonjwa yasioambukiza ikiwemo Kisukari na viashiria vyake kwa ujumla” amesema Dkt. Rusibamayila.

Amesema kuwa watanzania wengi hawana budi kujikinga na ugonjwa huo kwani ni watu asilimia 60 hufariki kwa ugonjwa huo duniani kwa kila mwaka.

Aidha, kwa mujibu Wa Dkt. Rusibamayila amesema kuwa asilimia kubwa ya wanawake nchini wana uzito mkubwa,mafuta mengi na hawajihusishi na mazoezi hivyo hupelekea kupata athari za ugonjwa wa kisukari.

Hata hivyo, ameongeza kuwa licha ya kufanya mazoezi lakini pia wanatakiwa kuepuka matumizi ya vileo kama vile uvutaji tumbaku,unywaji pombe na uvutaji wa shisha ili kuepuka magonjwa yasioambukiza kwani yamekuwa hatari kwa watanzania.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha chakula na Lishe (TFNC) Dkt. Vicent Assey amesema kuwa sambamba na kufanya mazoezi watanzania wanatakiwa kuzingatia mlo ulio bora ili kuepuka ugonjwa wa kisukari.

 

Lema ataka wabunge wa CUF waondolewe Bungeni
Magazeti ya Tanzania leo Novemba 12, 2017